Wakati wa pasaka, Wafuasi  wa Kristo hujikuta  katika Siri kubwa.  Siri iletayo hofu. 

Tunatafakari Siri inayojaza mioyo yetu na maajabu, upendo, na sifa. Tunakiri kwamba Siri hiyo ni zaidi ya uwezo wetu wa kueleza kwa akili ya kibinadamu kuelewa. Japokuwa kutokana na ushuhuda wa uhakika na furaha, tunaisherekea kama kumbukumbu takatifu na tumaini tukufu. 

Yeye  aliyefia  Kalvari ni nafsi  ya pili katika utatu mtakatifu. Ni Mungu ambaye tunakumbuka  kujitoa kwake  tunapozungumzia Msalaba.  Ni yeye yule wa milele ambaye ameinamisha kichwa kwa maumivu pale mlima Kalvari. Yeye anayefia Kalvari ni Mungu. 

Mungu tunayemtumikia ni Mungu wa milele, yeye aliyekuwepo kabla ya wakati,  anaishi ndani ya wakati na ataendelea kuwepo hata baada ya wakati kutoweka. Huyu ndiye Mungu ambaye milango ya kifo haiwezi kumzuia. Yeye aliyesulubishwa na kulazwa ndani ya kaburi  iliyoazimwa sio tu Muumbaji na mwenye kutoa uzima, ila ndiyo huo uzima. 

Yeye aliyejitambulisha kama “njia, kweli na uzima,” hupulizia pumzi mpya ya uzima ndani ya uzima wetu wa kale unaotufanya tupate kuzaliwa upya. Bwana ambaye ndiye “uzima” hutamka uzima katika vifo vyetu na kuleta pumzi ya upya wa maisha pale ambapo njia za kale na vifungo vyake vinaendelea kuathiri na kudhoofisha wasafiri katika safari ya uzima. 

Mungu wa Pasaka ndiye Baba ambaye ndani ya Yesu Kristo aliachana na mahali palipotayarishiwa wafu, akafungua Mlango wa kutoka mautini kwenda kwenye uzima na, moja kwa moja akashinda jinamizi la kifo lenyewe. Ndiyo sababu tunashangilia kwa ushindi: “Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchugu wako?” Na tunatamka wazi:  “Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo” (Wakorintho 15:55&57- Swahili Bible-UV).

Tunapotamka kwamba “Yesu amefufuka” amefufuka kweli kweli.  Tunahadithia siri ya utatu wa Mungu anayetutengenezea njia katika ukame wa jangwa la siku zetu. Mungu huwaleta watu kwa muumba na Mwokozi wao na kuwekeza ndani yao zawadi ya uzima tele, ambayo ina nguvu sana kiasi kwamba kifo hakiwezi kuondoa. Huu ndiyo uzima ujao ambao unajidhihirisha kwa kupandikizwa ndani ya uwezo wetu  wa kila siku. 

Mungu wa utatu na maajabu anapanda mlima Kalvari, anatoa uhai wake ili tupokee uzima, na tena kuchukua huo uzima tena na kujenga ngome ya matumaini ambamo ndani yake wanadamu wanaweza kupata tumaini ambayo  ulimwengu hauwezi kuwapatia. 

Tunaposherekea Pasaka, tunadhihirisha tumaini la uhakika kwamba Kristo alifufuka anaishi ndani yetu kama vile na sisi tulivyo ndani yake. Maisha yetu sio ya kawaida kama yale yaliyonaswa katika siri ya maisha inayotawala katikati ya kuzaliwa na kufa. Wala sio maisha ya hatari yasiyo na furaha ya milele. Wakati wa Pasaka, tunasherekea zawadi ya uzima wa milele inayopatikana kutokana  na kufa na kufufuka kwa Mwana wa Mungu. Haleluya! 

Neville Callam
Katibu Mkuu
Baptist World Alliance

(Maelezo katika Kiswahili na Harrison G. Olan’g)